Wachezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa wakiwashukuru mashabiki wao.
Katika mchezo huo wenyeji wa michuano ya mataifa ya Ulaya Euro 2016 inayoendelea nchini Ufaransa timu ya taifa ya Ufaransa usiku wa kuamkia hii leo wamefanikiwa kukata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kuichapa timu ya Iceland kwa jumla ya magoli 5-2.
Kwa ushindi huo sasa timu ya taifa ya Ufaransa inaungana na timu nyingine za Ureno, Wales, mabingwa wa dunia Ujerumani katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ambapo michezo yake itapigwa katikati ya juma hili.
Katika mchezo huo Ufaransa ambayo ilicheza mchezo huo kwa kasi na kudhamiria ushindi huo mapema magoli yake yalifungwa na Olivier Giroud aliyepachika mawili 2 katika dakika ya 13 na 59, lingine likifungwa dakika ya 20 na kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Paul Pogba, na dakika 2 baadaye kunako dakika ya 45 Dimitri Payet akapachika lingine huku Antonie Griezmann akifunga dakika ya 43 .
Magoli yakufutia machozi kwa upande wa Iceland yamepachikwa na Kolbeinn Sigthorsson katika dakika ya 58 na dakika ya 84 Birkir Bjarnason alifunga bao la pili lakufutia machozi.
Nusu fainali ya michuano hiyo itapigwa katikati ya wiki hii ambapo Ureno wao watavaana na timu ya Wales huku wenyeji Ufaransa watakuwa na kibarua kizito mbele ya mabingwa wa dunia timu ya taifa ya Ujerumani.