Ijumaa , 26th Apr , 2019

Shirikisho la soka nchini TFF, limewaondoa kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu msimu huu waamuzi watatu waliochezesha mchezo wa KMC na Simba jana April 25, 2019.

Wachezaji wa Simba na KMC pamoja na Mwamuzi Abdallah Kambuzi

Waamuzi hao ni Abdallah Kambuzi, Godfrey Msakila na Consolata Lazaro, ambao wametajwa kuchezesha chini ya kiwango.

Taarifa ya TFF imeeleza kuwa sababu ya kuwaondoa ni kuonesha kiwango kisichoridhisha hivyo kukosa sifa za kuendelea kuchezesha.

Katika mchezo huo mwamuzi Abdallah Kambuzi ndio alikuwa refarii wa kati huku Consolata na Msakila wakiwa wasaidizi.

Mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba, ulimazika kwa Simba kushinda mabao 2-1 huku ikipata penalti mbili ambayo moja alikosa Meddie Kagere huku nyingine ikifungwa na John Bocco.

Pia kunaa matukio kadhaa ambayo yalilalamikiwa ikiwemo KMC kunyimwa penalti pamoja na nafasi ya kufunga goli kwa mwamuzi kupuliza kuwa mchezaji amezidi ikiwa ni mpira wa kurudishwa na beki ambao kisheria za soka hauwezi kuwa na tendo la kuotea.