Jumatano , 13th Jan , 2016

Timu ya URA ya Uganda imetwaa ubingwa wa kombe la Mapinduzi katika mchezo wa fainali uliomalizika hivi punde katika dimba la Amaan visiwani Zanzibar.

Timu ya URA ya Uganda imetwaa ubingwa wa kombe la Mapinduzi katika mchezo wa fainali uliomalizika hivi punde katika dimba la Amaan visiwani Zanzibar.

URA imepata ubingwa huo wa mashindano ya 10 yenye lengo la kuadhimisha siku ya mapinduzi ya Zanzibar kwa kuifunga Mtibwa Sugar kutoka Tanzania bara jumla ya mabao 3 kwa 1.

URA ilianza kufunga katika dakika ya 16 ya mchezo kupitia kwa Julius Ntambi na hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Mtibwa ilikuwa nyuma kwa bao hilo.

Kipindi cha pili kilianza kwa Mtibwa kushambulia kwa kasi wakitafuta bao la kusawazisha lakini mambo yakawa tofauti kwani dakika ya 85 Peter Lwasa aliweza kuipatia URA bao la pili.

Wakati Mtibwa wakitafakari, Peter Lwasa tena akafunga bao la tatu na kuzima kabisa ndoto za Mtibwa licha ya kupata bao la kufutia machozi katika dakika za nyongeza kupitia kwa Jafari Salum.

Licha ya kufungwa, Mtibwa wamemiliki asilimia 51 ya mchezo huku URA ikimiliki mchezo kwa asilimia 49.

Nahodha wa mtibwa Shaaban Nditi amekubali matokeo na kuwapongeza URA huku akijutia kosa ambalo wamelifanya kipindi cha kwanza na kusababisha wao kufungwa bao lililowafanya washambulie zaidi kipindi cha pili huku wakisahau kujilinda.

Mabingwa wapya wa kombe hilo ambalo lilikuwa likishikiliwa na Simba, URA wamekabidhiwa kombe pamoja na kitita cha shilingi za kitanzania Milion 10, huku Mtibwa wakiambulia shilingi milioni 5 za kitanzania.

Katika mashindano ya mwaka huu, URA waliokuja kama timu waalikwa wameruhusiwa kuondoka na kombe tofauti na miaka ya nyuma ambapo timu kutoka nje ya Tanzania haikuruhusiwa kuondoka kombe, jambo ambalo limewahi kuwakuta KCCA ya Uganda.