Jumatano , 24th Nov , 2021

Beki kitasa, Sergio Ramos huenda akacheza mchezo wake wa kwanza akiwa na timu yake ya PSG baada ya kujuimshwa katika kikosi kitakachocheza dhidi ya Manchester City saa 5:00 usiku wa leo Novemba 24, 2021 kwenye michuano ya Klabu bingwa barani Ulaya 'UCL'.

(Beki wa PSG, Sergio Ramos akiwa mazoezini)

Gwiji huyo wa Real Madrid, hajacheza mchezo wowote wa kiushindani tokea ajiunge na matajiri hao wa jiji la Paris nchini Ufaransa mwezi Agosti mwaka huu kutokana na kuwa na majeraha ya muda mrefu.

Ramos alikuwa kwenye benchi katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Nantes Jumamosi ya Novemba 20, 2021 lakini kocha wake Mauricio Pochettino hakumchezesha kwasababu inayoelezwa hakutaka kumuharakisha mkongwe huyo.

Iwapo atapata dakika zozote dhidi ya kikosi cha Pep Guardiola basi utakuwa mchezo wake wa kwanza tokea Mei 5, 2021 alipokuwa Real Madrid ilipocheza dhidi ya Chelsea na Madrid kupoteza kwa 2-1 na Chelsea  kwenye nusu fainali ya UCL.

Manchester City ndiyo kinara wa kundi A akiwa na alama 9, akifuatiwa na PSG mwenye alama 8, Clubb Brugge watatu akiwa na alama 4 wakati RB Leipzig anashika mkia akiwa na alama 1. PSG na City yeyote atafuzu hatua ya 16 bora ya UCL endapo akipata ushindi.