Alhamisi , 19th Mar , 2015

Wachezaji wa timu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars wametakiwa kucheza kwa bidii ili kuweza kujipatia soko la soka katika timu mbalimbali za nje ya nchi.

Akizungumza jijini Dar es salaam wakati wa kukabidhi bendera ya nchi kwa timu hiyo inayotarajiwa kuondoka kesho kuelekea nchini Zambia, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini TFF, Mwesigwa Celestine amesema, soka la wanawake hivi sasa limepanda hivyo wachezaji hao wana nafasi kubwa ya kupata timu za nje ambazo ni nafasi nzuri kwa upande wao na kwa taifa kwa ujumla.

Mwesigwa amesema, wachezaji hao wanatakiwa kucheza kwa kuamini wanashindana na sio kushiriki katika mechi dhidi ya timu ya Taifa ya Wanawake ya Zambia siku ya Jumapili ili kuweza kuipigania timu pamoja na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Kocha wa Timu hiyo, Rogasian Kaijage amesema, anaamini atashindana na kushinda kutokana na mabadiliko ya kikosi chake cha mwaka jana na mwaka huu.

Kwa upande wake, Nahodha wa Timu hiyo, Sophia Mwasikili amesema anawaamini wachezaji wenzake na watakuwa na ushirikiano pamoja na kuzingatia mazoezi ya kocha ili waweze kuibuka na ushindi katika mechi hiyo dhidi ya Zambia.

Twiga Stars inaanzia hatua ya pili katika kuwania kufuzu kwa Fainali za Afrika kwa Wanawake baada ya kuwa katika nafasi za juu kwa viwango barani Afrika na endapo itafanikiwa kuwaondoa Wazambia itafuzu moja kwa moja kwa fainali hizo.

Msafara wa Twiga Stars utaongozwa na na Blassy Kiondo ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Beatrice Mgaya kiongozi msaidizi, Rogasin Kaijage kocha mkuu, Nasra Juma (kocha msaidizi), Furaha Francis (Meneja), Christine Luambano (Daktari) na Mwanahamis Abdallah (Mtunza vifaa).

Wachezaji watakaokweda Zambia ni Asha Rashid, Mwajuma Abdallah, Mwanahamis Omar, Donisi Minja, Amina Bilal, Fatuma Bashiri, Esther Chabruma, Shelda Mafuru, Maimuna Kaimu, Najiat Abbas, Stumai Abdalla, Fauma Issa, Thereza Yona, Fatuma Hassan, Fatuma Omary, Sophia Mwasikili, Fatuma Khatibu na Etoe Mlenzi.