Jumatano , 20th Mei , 2015

Timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars inatarajiwa kuingia kambini katika wiki ya pili ya mwezi Juni kujiandaa na michuano ya All African Games inayotarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu nchini Congo Brazzavile.

Akizungumza na East Africa Radio, katibu mkuu wa shirikisho la soka nchini TFF, Mwesigwa Celestine amesema, timu hiyo itakaa kambini kwa muda wa siku 10 na baada ya hapo watakuwa na mechi mbalimbali za majaribio, na baadaye watapumzika kwa, muda wa wiki mbili na watarudi tena kambini kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kwa ajili ya kushiriki michuano hiyo.

Mwesigwa amesema, timu hiyo inahudumiwa lakini kwa gharama za Programu nyingine zikiwemo za vijana, waamuzi na makocha ambapo suala hilo linaendelea kurudisha nyuma maendeleo ya soka la wanawake nchini.

Mwesigwa amesema, wadhamini wanatakiwa kujitokeza kwa ajili ya kusaidia timu hiyo ili kambi iweze kuwa nzuri na timu kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuitangaza nchi katika ramani ya michezo.