Wanamichezo Olimpiki iliopita wa Tanzania katika picha nchini Uingereza.
Kamati ya Olimpiki Tanzania TOC imeanika kikosi cha wanamichezo 12 watakaokwenda kushiriki michuano ya michezo ya Olimpiki itakayoanza Agasti 8 mwaka huu nakumalizika Agasti 21 mjini Rio nchini Brazil.
Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania Filbert Bayi amesema wanamichezo hao wote yaani kikosi kizima kitaondoka kwa makundi kutokana na kuchelewa kupata majina ya mwisho ya wanamichezo walioombewa nafasi maalumu za upendeleo baada ya kushindwa kufuzu na kusubiri nafasi hizo.
Bayi ambaye alikuwa mwanariadha bingwa na mshindi wa medali ya michuano mikubwa duniani amesema kundi la kwanza la timu hiyo litaongozwa na mkuu wa msafara Suleiman Jabir ambaye atatangulia kwa ajili ya kazi maalumu ya kuratibu masuala masuala muhimu ya timu hiyo ikiwa nchini Brazil ambapo moja ya kazi hiyo ni mapokezi ya kikosi hicho wakati kikiwasili mjini Rio tayari kwa michuano hiyo.
Kundi la pili litakuwa la wanamichezo wa mchezo wa kuogelea, judo, na baadhi ya wanariadha, dakatari wa timu Dk. Nassoro Matuzya ambao wote kwa pamoja wanataraji kuondoka nchini Agasti 2 mwaka huu, huku kundi la mwisho litakuwa la wanariadha wa marathon ambao ambao wataondoka Agasti 16 kwa sababu wao watakimbia Agasti 21 hivyo mwalimu wao aliandika barua kuomba waendelea kubakia nchini ili kufanya maandalizi zaidi kuliko kwenda mapema na pengine wasipate nafasi ya kufanya hivyo kwa utulivu kwa kuwa tayari michezo itakuwa imeshaanza rasmi.
Aidha, Bayi akalazimika kufafanua kuwa wanamichezo amaanishi wachezaji pekee wa michezo kiwanjani bali idadi hiyo inajumuisha pia watu wengine kama makocha, viongozi na daktari ndio ambao watakwenda kuiwakilisha nchi katika michuano hiyo.
Akimalizia Bayi amewataja wanamichezo hao akianza na wanariadha wa mbio za marathon ambao wataenda katika michuano hiyo pamoja na Fabian Joseph, Alphonce Felix, Said Makula, Sara Ramadhan na wataambatana na kocha wao Francis John.
Wanamichezo wengine ni wa mchezo wa kuogelea ambapo Hilal Hemed Hilal na Magdalena Mushi watashiriki kuogelea mita 50 miondoko huru [free style] wao wakishiriki kwa nafasi za upendeleo na wataambatana na kocha wao Alexander Mwaipasi huku mchezo wa Judo wakiwakilisha na Andrew Thomas Mlugu atakayecheza uzito wa kilo 73 ambapo pia ataambatana na kocha wake Zaidi Hamis Omar.
Msafara wa kikosi hicho cha wanamichezo wa Olimpiki wa Tanzania kitaongozwa na mkuu wa msafara Suleiman Mahamood Jabir na Daktari wa timu hiyo atakuwa Nassoro Ally Matuzya.
Akimalizia Bayi ameongeza kusema kuwa kuna Watanzania wengine watakwenda katika michuano hiyo kutokana na nafasi zao na kimsingi hao hawatakuwa sehemu ya timu ambapo katika watu ambao watakwenda kwa nafasi zao ni pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye, Rais wa TOC Ghuram Rashid na Katibu Mkuu wake Filbert Bayi.