Ijumaa , 2nd Jan , 2015

Chama cha Gofu Tanzania TGU kinatarajia kufanya uchaguzi mkuu wa viongozi Machi 6 mwaka huu baada ya uongozi uliopo madarakani kumaliza muda wake mwezi ujao.

Akizungumza na East Africa Radio, Katibu Mkuu wa TGU, Joseph Tango amesema mchakato wa uchaguzi huo unatarajiwa kuanza mwezi huu ili chama kiweze kupata viongozi watakaoendeleza juhudi za mchezo huo zilizoanzishwa na uongozi utakaomaliza muda wao wa kukaa madarakani.

Tango amesema uongozi unaotarajiwa kuondoka madarakani umeanzisha programu mbalimbali zitakazoufanya mchezo huo kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, hivyo unahitaji kukabidhi madaraka kwa uongozi mpya mwanzoni mwa mwaka huu ili ziweze kutekelezwa mapema na kuleta matunda yaliyokusudiwa.

Tango amesema timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 18 imeandaliwa kwa muda wa miaka miwili na kuna programu ya muda mrefu ambayo inatakiwa kukabidhiwa mapema kwa uongozi mpya ili iendelezwe kwani kucheleshwa kukabidhiwa kuchangia kushusha viwango vya wachezaji.