Jumanne , 24th Nov , 2015

Shirikisho la soka nchini TFF limesema, chama cha soka mkoa wa Dar es salaam DRFA inatakiwa kuchukua hatua katika mgogoro wa uchaguzi uliopo katika chama cha mpira mkoa wa Temeke TEFA.

Katibu Mkuu wa TFF Mwesigwa Celestine amesema, DRFA inatakiwa kuhakikisha inalinda kanuni na sheria za mpira hususani katika suala la kupeleka mgogoro wa soka mahakamani.

Mwesigwa amesema, DRFA wanatakiwa kuhakikisha wanaingilia kati mgogoro huo na kutoa onyo juu ya mgogoro wa soka kupelekwa mahakamani na ikishindikana wahusika wawajibishwe kisheria na sio kulalamika wakati nguvu zipo katika dawati lao.

Mgogoro wa TEFA unatokana na uchaguzi wa viongozi uliofanywa kimyakimya licha ya kuwepo na amri ya mahakama kusitisha uchaguzi huo usiendelee kutokana na mmoja wa wagombea wa nafasi katika uchaguzi huo kufungua mashtaka dhidi ya viongozi wanaosimamia uchaguzi huo.

Mahakama ya Temeke ilizuia uchaguzi huo baada ya kufunguliwa kwa shauri dhidi ya mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya TEFA, Mwenyikiti wa kamati ya uchaguzi ya DRFA na mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya TFF.

Mwenyekiti wa uchaguzi wa TEFA Rashid Salada alikiri kupokea taarifa kutoka mahakama ya Temeke inayozuia uchaguzi huo usifanyike Novemb 22 mwaka huu kutokana na kuwepo kwa shauri mahakamani linalohusu uchaguzi huo.