Jumamosi , 5th Apr , 2014

Timu ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania imefanikiwa kuingia nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Dunia yanayofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil baada ya kuifunga Indonesia kwa jumla ya mabao 5-3.

Timu ya taifa ya Tanzania ya watoto wa mitaani

Timu ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania imefanikiwa kuingia nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Dunia yanayofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil baada ya jana kuifunga Indonesia kwa jumla ya mabao 5-3.

Hadi muda wa kawaida wa mchezo huo unamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2 ndipo ikatumia mikwaju ya penalti kuamua mshindi. Tanzania ilipata penalti tatu dhidi ya moja ya wapinzani wao.

Kwa matokeo hayo, Tanzania sasa itacheza mechi ya nusu fainali leo dhidi ya Marekani ili kupata timu zitakazocheza mechi za fainali na kutafuta mshindi wa tatu. Mechi za fainali na kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa kesho (Aprili 6 mwaka huu).
Timu nyingine zilizoingia nusu fainali na mechi zake zinachezwa leo (Aprili 5 mwaka huu) ni Burundi itakayocheza na Pakistan.

Katika mechi zilizopita, Tanzania ilitoka sare ya mabao 2-2 na Burundi, ikaitandika Argentina mabao 3-0 ikailaza Nicaragua mabao 2-0 na ikafungwa na Philippines mabao 2-0.