Jumanne , 17th Nov , 2015

Timu ya Taifa ya Tanzania leo usiku saa 1:15, sawa na saa 3:15 kwa saa za Afrika Mashariki itashuka Uwanja wa Mustapher Tchaker dhidi ya Algeria katika mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu kwa fainali za kombe la Ddunia mwaka 2018 nchini Urusi.

Kocha mkuu wa Taifa Stars Charles Boniface Mkwasa amesema anashukru vijana wake wote wapo salama, hakuna majeruhi kikubwa anachosubiri ni jioni kushuka uwanjani kusaka ushindi katika mchezo huo.

Kwa upande wake, mchezaji wa zamani ambaye pia ni kocha msaidizi wa Timu ya Tanzania Bara The Kilimanjaro Stars Juma Mgunda amesema, wana imani Stars ina uwezo mkubwa wa kufanya vizuri kwani wanajua majukumu yao ni yapi kwa ajili yao na nchi kwa ujumla.

Mgunda amesema, kubwa lililobakia ni kumalizia kazi iliyobakia japo walishindwa kufanya nyumbani lakini mpira unachezwa popote na Stars ina uwezo wa kufanya vizuri na kuweza kusonga mbele.

Kwa upande mwingine mdau wa soka Masau Bwire amesema, wachezaji wakihimizana na kujua ni kitu gani wanakihitaji kufanya kwa ajili ya Tanzania basi uwezo wa kuweza kuifunga Algeria upo.

Stars inashuka dimbani kusaka ushindi katika mchezo wa leo, utakaoipelekea kuweza kusonga mbele kwa hatua ya makundi, kufuatia kutoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Novemba 14 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.