Jumapili , 1st Jun , 2014

Wakicheza kandanda safi wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania taifa stars wameweza kuwatoa kimasomaso watanzania baada ya hii leo kutinga hatua ya pili ya michuano ya mtoano kusaka tiketi ya kucheza fainali za Afrika.

Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania taifa stars ambacho kimeitoa timu ya taifa ya Zimbabwe.

Timu ya taifa ya Tanzania taifa stars imefanikiwa kutinga hatua ya pili ya mtoano wa kuwania tiketi ya kucheza michuano ya Afrika CAN itakayopigwa mwakani nchini Morocco baada ya hii leo kuiondoa timu ya taifa ya Zimbabwe ugenini kwa jumla ya mabao 3-2 .

Matokeo hayo yanafuatia sare ya mabao 2-2 huko jijini Harare nchini Zimbwabwe na awali stars iliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam kwa goli pekee lililofungwa na mshambuliaji mrefu John Bocco.

Katika mchezo wa hii leo uliofanyika katika uwanja wa Rufaro jijini Harare magoli ya Stars yalifungwa na beki kisiki Nadir Haroub ‘canavaro’ likiwa la kusawazisha baada ya awali Zimbabwe kupata bao la kuongoza kupitia kwa Danny Phiri.

Na mwanzoni mkwa kipindi cha pili mshambuliaji mwenye nguvu nyingi uwanjani Thomas Ulimwengu akaipa uongozi stars kwa goli la pili ambalo baadae wazimbabwe walisawazisha kupitia kwa kiungo mshambuliaji wao Willard Katasande.

Kwa matokeo hayo sasa stars itavaana na msumbiji katika hatua ya pili ya michuano hiyo na mshindi ataingia katika hatua ya makundi.