Alhamisi , 3rd Dec , 2015

Katika kuboresha kikosi chake kwa ajili ya kuelekea katika muendelezo wa michuano ya ligi kuu ya soka Tanzania Bara, uongozi wa Stand United ya mkoani Shinyanga imefanikiwa kunasa saini ya beki kutoka Ivory coast, Assouman N'guessan David

Msemaji wa timu ya Stand United Deo Makomba amesema beki huyo amesaini mkataba wa miaka miwili akitokea klabu ya Olympique Sports Abobo ya Ivory Coast.

Makomba amesema uamuzi wa kusajili mchezaji huyo unatokana na mapendekezo ya benchi la ufundi la timu hiyo na wanaamini ujio wake utaimarisha safu ya ulinzi ya Stand United huku wakitarajia kufunga usajili kwa kusajili wachezaji wengine wawili wa hapa nchini.

Kwa upande mwingine, uongozi wa Stand United umewatoa kwa mkopo wachezaji wake watatu kwenda Polisi Tabora ambao ni Heri Khalifa, Khalid Suleiman na Rashid Magona wakati Jisendi Mathias amepelekwa Geita Gold Mine FC huku Hamad Ndikumana, Hamad Manzi, Shabani Dunia na John Mwenda wakiachwa na timu hiyo na kuwa wachezaji huru.