Jumatatu , 19th Jul , 2021

'Sports Countdown' ya East Africa redio inakupitisha kuangazia stori sita kali za michezo kitaifa na kimataifa kwa mtindo wa kuzihesabu kuanzia nambari 6 hadi 1 huku kila namba ikiwa imebeba mahusiano muhimu na stori yenyewe.

Kikosi cha Simba kikisheherekea Ubingwa wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara kwa msimu wa mwaka 2020-2021.

6 – Ni idadi ya wacheza tenisi nyota Duniani wanaotazamiwa kukosekana kwenye michuano ya Olympic inayotaraji kufanyika kuanzia Julai 23 na kutamatika Agosti 8 mwaka huu kwenye Jiji la Tokyo nchini Japan kutokana na sababu mbalimbali.

Orodha ya wachezaji hao inazidi kuwa ndefu na hii ni mara baada ya mcheza tenisi chipukizi wa nchini Marekani, mwanadada Coco Gauff mwenye umri wa miaka 17 kupatwa na maambukizi ya Covid-19 na kuondolewa kwenye mashindano hayo.

Coco anayeshika nafasi ya 25 kwa ubora Duniani kwa upande wa wanawake wacheza tenisi, anaungana na nyota wengine watakaokosekana kwa sababu mbalimbali ikiwemo Covid-19 ikiwemo mwanamama, Serena Williams, Johanna Konta, Simona Halep, Naomi Osaka na Angelique Kerber kwa upande wa wanawake pekee.

Kwa upande wa wanaume, watakaokosekana ni Rodger Federer, Rafael Nadal, Dominic Thiem na Ben Davies.

5 – Ni idadi ya miaka aliyosaini mshambuliaji chipukizi raia wa Albania, Armando Broja kuendelea kusalia kwenye klabu yake ya Chelsea hadi mwaka 2026 baada ya kumaliza mkataba wake wa mkopo na klabu ya Vitesse ya nchini Uholanzi na ambapo aliichezea michezo 34 na kufunga mabao 11.

Inaelezwa uamuzi wa kumuongezea kandarasi kinda huyo umekuja baada ya mshambuliaji mkongwe, Olivier Giroud kutimkia AC Milan ya Italia na kusaini kandarasi ya miaka miwili na mabingwa hao wa zamani wa klabu bingwa Ulaya.

4 – Ni idadi za timu zilizoshuka daraja moja kwa moja kutoka Ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu wa mwaka 2020-2021 kufuatia kuwa na mwenendo wa matokeo yasiyoridhisha, vilabu hivyo ni Mwadui kutoka mkoani Shinyanga, Ihefu kutoka Jijini Mbeya, Gwambina ya Jijini Mwanza na Maafande wa JKT Tanzania ya Dar es Salaam.

Coastal Unio iliyomaliza kwenye nafasi ya 14 itacheza michezo ya mtoano kuwania kutokushuka daraja ugenini dhidi ya Pamba ilhali Mtibwa Sukari iliyomaliza kwenye nafasi ya 13 itachuana na Transit Camp ugenini, michezo yote ya mzunguko wa kwanza itapigwa Julai 21 mwaka huu na kurudiana Julai 24 wakati Mbeya Kwanza ya Mbeya na Geita Gold ya Geita zimepanda moja kwa moja kucheza ligi kuu baada ya kuwa vinara wa kundi A&B.

3 – Ni idadi ya michezo iliyopat aushindi timu ya Milwaukee Bucks mbele ya Phoenix Suns kwenye fainali ya ligi ya kikapu nchini Marekani NBA na hii ni mara baada ya kuibuka na ushindi wa alama 123-119 mbele ya Suns alfajiri ya jana kwenye mchezo watano wa fainali hiyo hivyo kuhitaji ushindi kwenye mchezo mmoja tu ili kuwa mabingwa wapya wa NBA msimu huu.

Wawili hao watashuka dimbani tena Julai 21 mwaka huu kukipiga kwenye mchezo wasita utakaotoa taswira yakumsaka bingwa hadi mchezo wa mwisho wa saba ama laa.

2- Ni idadi ya timu zinazowania kumsajili kiungo nyota wa klabu ya Sassoulo na timu ya taifa ya Italy, Manuel Locatelli, vilabui hivyo ni washika mitutu wa jiji la London, timu ya Arsenal ambao wapo tayari kutoa paundi milioni 40 za England ambazo ni sawa na bilioni 120 za kitanzania na Juventus ya Italy klabu ambayo nyota huyo inaelezwa amefunguka kuwa angependa kujiunga nayo badala ya Arsenal.

Locatelli aliyecheza michezo 34 amefunga mabao 4 na kutengeneza mabao 3 anavitoa udenda vilabu vya ulaya baada ya kuonesha kiwango kizuri kwenye michuano ya UEFA EUROS na kuchangia Italy kuibuka kuwa mabingwa.

1 – Ni nafasi aliyoshikilia klabu ya Simba na kumuwezesha kuwa bingwa wa Ligi kuu nchini VPL ambapo jioni ya jana aliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Namungo ya mkoani Lindi na kufikisha alama 83 utofauti wa alama 9 na makamu bingwa watano wao wajadi, Klabu ya Yanga ambayo ililazimishwa sae ya bila kufungana na Dodoma Jiji jijini Dodoma.

Baada ya mchezo wa Simba kumalizika, mabingwa hao mara nne mfululizo walikabidhiwa kombe na aliyekuwa mgeni rasmi wa tukio hili maalum, mheshimiwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala na kubariki sherehe za ubingwa kwenye dimba la Mkapa jijini humo.

Simba na Yanga zitaiwakilisha nchi kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika ilhali Azam na Biashara United Mara zitacheza michuano ya Shirikisho Afrika kwa msimu ujao wa mwaka 2021-2022.