
Mjamaica, Elain Thompson-Herah akisheherekea ushindi wa mitaa 200 za wanawake kwenye michuano ya Olympic inayoendelea nchini Japan.
6 – Ni idadi ya magoli aliyoyafunga kiungo mkata umeme wa klabu ya Liverpool, Mbrazil Fabinho kwenye michezo 86 aliyoicheza kwenye ligi kuu ya England pekee tokea ajiunge na majogoo hapo wa jiji Julai 2018 akitokea klabu ya AS Monaco ya nchini Ufaransa.
Mkali huyo wa kutibua mashambulizi ya wapinzani amesaini kandarasi ya miaka mitano usiku wa kuamkia leo kuendelea kusalia na mabingwa hao wa msimu juzi wa michuano ya klabu bingwa barani ulaya hadi mwaka 2026.
5 – Ni idadi ya miaka iliyopita tokea timu ya taifa wa mpira wa kikapu ya nchini Marekani itwae ubingwa wa michuano ya Olympic iliyofanyika nchin Brazil kwa kuifunga timu ya taifa ya Serbia na kubeba medali za dhahabu mara 15 na kuendelea kuwa bingwa wa kihistoria ya michuano hiyo katika mara 18 alizoshiriki.
Wababe hao wanataraji kukipiga dhidi ya Australia siku ya kesho saa 1:15 asubuhi kwenye dimba la Saitama kwenye nusu fainali ya kwanza ilhali Ufaransa na Slovenia zitakutana kwenye mchezo wa nusu fainali ya pili itakayochezwa saa 8:00 mchana siku hiyo hiyo ya Agosti 5, 2021.
4 – Ni nafasi inayoshika timu ya Atlabara kutoka Sudan Kusini na kushika mkia kwenye kundi A la michuano ya CECAFA KAGAME CUP baada ya kucheza mchezo mmoja na kufungwa na bao 1-0 na mabingwa wa Uganda, timu ya Express kwenye mchezo wake wa kwanza.
Wababe hao wa Sudan Kusini wanataraji kujiuliza kwenye mchezo wake wapili wa kundi A utakaochezwa saa 1:00 usiku wa leo Agosti 4, 2021 dhidi ya timu ya wananchi, klabu ya Yanga iliyomsajili Mshambuliaji wake wa zamani Heritier Makambo kwa kandarasi ya miaka miwili.
Mchezo mwingine wa michuano hiyo utakaocheza hii leo, ni ule wa saa 10:00 jioni ambapo Nyasa Big Bullets ya Malawi itachuana na Express ya Uganda.
3 – Ni idadi ya miaka ambayo mshambuliaji wa sasa wa Inter Milan, Romelu Lukaku mwenye umri wa miaka 28 alidumu kwenye klabu ya Chelsea kuanzia msimu mwaka 2011-2014 kwa kucheza michezo 15 pekee na hatimaye kuuzwa kwenye klabu ya Everton ya nchini England akiwa bwana mdogo mwenye umri wa miaka 21.
Taarifa zinaripoti kuwa Chelsea imedhamiria kutaka kumsajili tena mkali huyo wa kupachika mabao kwa sasa na tayari wamepeleka ofa mbili zilizopigwa chini na Inter Milan huku Chelsea ikitaraji kujipanga upya na kupeleka ofa ya paundi Milioni 100 sawa na zaidi ya bilioni 300 za Kitanzania pamoja na Chelsea kuwa tayari kumtoa Marcos Alonso kwenye dili hilo.
2 - Ni idadi ya tuzo za mchezaji bora wa ligi ya kikapu nchini Marekani NBA MVP alizoshinda Nyota wa Golden State Warriors, Stephen Curry katika msimu wa mwaka 2015 na 2017.
Nyota huyo yupo nchini Tanzania na ametembelea hifadhi ya Serengeti akiwa na mke wake wakisheherekea kutimiza miaka 10 ya ndoa yao. Stephen Curry anakuwa nyota watatu kutoka tasnia ya michezo kutembelea hifadhi mbalimbali nchini kipindi cha hivi karibuni baada ya wanasoka Mohamed Sakho na Crystian Benteke wote kutoka klabu ya Crystal Palace ya England kutembelea Hifadhi ya ngorongoro mkoani Arusha.
1 – Ni idadi ya medali ya fedha aliyoshinda mwanariadha Mjamaica, Elain Thompson-Herah mwenye umri wa miaka 29 baada ya kushika nafasi ya mshindi wapili kwenye michuano ya mbio za urefu wa mita 400 za wanawake kwenye Olympic ya mwaka 2016 nchini iliyofanyika Rio de janeiro nchini Brazil.
Elain Thompson-Herah amezidi kuwa gumzo mara baada ya kuwa mshindi wa kwanza kwenye mbio za urefu wa mita 100 na mita 200 za wanawake na kupata medali mbili za dhahabu na kuweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kutetea medali zako mbili za dhahabu za mbio hizo kwa pamoja baada ya kushinda kwenye Olympic ya mwaka 2016 nchini Brazil.
Elain alishinda mbio za mita 200 baada ya kukimbia kwa kasi kwa kutumia sekunde 21.53 na kuweka rekodi ya kuwa mwanamke wa pili kwenye historia ya mbio za umbali huo kwa upande wa wanawake rekodi inayoshikiliwa na Griffith Joyner aliyetumia sekunde 21.34 mwaka 1988.