Sports Countdown Julai 16, Fei Toto aweka rekodi

Ijumaa , 16th Jul , 2021

Stori sita (6) za michezo (Sports Countdown) leo asubuhi kwenye Supa Breakfast ya East Africa Radio kuanzia Saa 1:15 Asubuhi, ambapo kila stori inatokana na namba 1 mpaka 6. Na moja ya stori kubwa leo ni Fei Toto avunja rekodi yake ya kufunga Yanga.

Fei Toto

6. Ni idadi ya michezo mipya itakayo Tambulishwa kwa mara ya kwanza kwenye michezo ya Olympic mwaka huu huko Tokyo, Japan kuanzia Julai 23 mpaka Agosti 8, 2021. Miongoni mwa michezo hiyo mipya ni pamoja na Kuteleza kwenye skateboard, Karate, Baseball na kuteleza kwenye maji (Surfing) na kufanya idadi ya michezo yote kufikia 33.

Jumla ya mataifa 206 ndiyo yatakayoshiriki mwaka huu huku jumla ya wanamichezo 11,238 na zaidi wanategemewa kushiriki.

 

5. Ni idadi ya watu waliokamatwa huko England kutokana na vitende vya ubaguzi wa rangi vilivyofanya na watu hao dhidi ya wachezaji watutu wa timu ya taifa ya England, wenye asili ya Afrika ambao ni Bukayo Saka, Jadon Sancho na Marcus Rashford.

Wachezaji hao walikutana na kadhia hiyo kupitia mitandao ya kijamii ya Tweeter, Facebook na Instagram baada ya kukosa penati kwenye mchezo wa fainali ya michuano ya Euro 2020, ambapo England ilifungwa na Italia kwa penati 3-2. Mamlaka za usalama nchini humo ziliahidi kufuatilia na kuwakamata watu wote waliofanya vitendo hivyo vya kibaguzi na chuki dhidi ya wachezaji hao. Na mchezaji Bukayo Saka kupitia mitandao yake ya kijamii aliandika kuonyesha hisia zake juu ya vitendo hivyo huku akisisitiza wasimamizi wa mitandao hiyo hawachukui hatua thabiti kusitisha vitendo hivyo.

 

4. Ni idadi ya timu zitakazoiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya vilabu barani Afrika msimu ujao kwenye klabu bingwa na kumbo la Shirikisho, na rasmi timu hizo zitakazo bebe bendera ya Tanzania kwenye michuano hiyo zimefahamika mara baada ya michezo ya roundi ya 33 ya VPL kuchezwa hapo jana na timu zilizomaliza katika nafasi nne za Juu kwenye msimamo kujulikana.

Timu hizo ni Vinara wa Ligi na Mabingwa wa VPL Simba Sc ambao wao watawakilisha kwenye michuano ya klabu bingwa sambamba na Yanga wanaoshika nafasi ya pili, wakati Azam FC walio nafasi ya tatu pamoja na Biashara mara United wao watashiriki michuano ya kombe la shirikisho.

 

3. Ni mataji ya Grandslams aliyoshinda mcheza tennis Angelique Kerber wa Ujerumani ambae ametangaza kutoshiriki katika michezo ya Olympic itakayo fanyika Tokyo Japan kuanzia julai 23 kwa kile alichodai anahitaji kuupumzisha mwili wake, hasa akizingatia kuwa na wiki kadhaa ngumu zilizipita ikiwemo kufika hatua ya nusu fainali kwenye michuano ya Wimbledon iliyomalizika wiki iliyopita.

Kerber mwenye umri wa miaka 33 ni mshindi wa Australian Open, US Open mwaka 2016 na Wimbledon mwaka 2018 anaungana na wacheza tenisi wengine kama Johanna Konta, Dan Evans, pamoja na mshindi mara 20 wa Grand Slam kwa wanaume Roger Federer. Ambao wato hawatashiriki kwa sababu tofauti tofauti.

2. Ni idadi ya mabao aliyofunga kiungo wa Yanga Feisal Salum maarufu Fei Toto kwenye mchezo wa Ligi kuu dhidi ya Ihefu hapo jana na kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, na kujihakikishia kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa VPL msimu huu wa 2020-21, ambapo Yanga imefikisha alama 73.

Mabao hayo yamemfanya fei Toto kufikisha mabao matano (5) msimu huu kwenye michezo 33 ikiwa ni idadi kubwa ya mabao aliyofunga ndani ya msimu mmoja tangu ajiunge na kikosi hicho msimu wa 2018-19 ambapo alifunga mabao manne (4), na msimu uliofata wa 2019-20 alifunga mabao mawili (2). Sasa Fei Toto ni wa moto

 

1. Nafasi anayoshikilia muendesha magari ya Langa langa F1 Max Verstappen wa timu ya Red Bull kwenye msimamo wa Dunia akiwa na alama 182 akiongoza kwa tofauti ya alama 32 dhidi ya bingwa mtetezi Lewis Hamilton anayeshika nafasi ya pili, na Dereva huyo raia wa Uholanzi amesema kuwa hana presha wala wasi wasi katika mbio hizo za ubingwa na amekuwa akijianda vizuri kuelekea kwenye kila mbio.

Verstappen amesema hayo alipokuwa akizungumzia maandalizi yake kuelekea kwenye mbio za England (British Grand prix) ambazo maandalizi yake yanaanza leo kwa mazoezi ya siku ya kwanza kabla ya mbio zenyewe kufanyika siku ya Jumapili Julai 18. Max Verstappen ameshinda kwenye mbio 5 kati ya 9 ikiwemo tatu zilizopita mfululizo.