Spika apiga kijembe Yanga, Tarimba akipokea

Alhamisi , 8th Apr , 2021

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeendelea leo Aprili 8, 2021, likiongozwa na Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai ambaye katika kipindi cha maswali na majibu alitupa kijembe kwa mbunge wa Kinondoni Abbas Tarimba kuhusu ushindi wa Simba SC.

Spika Job Ndugai na Mbunge Abbas Tarimba

Akimkaribisha kuuliza swali mbunge wa Kinondoni Spika Job Ndugai amesema kuwa Pasaka ya mwaka huu ilikuwa nzuri sana hasa baada ya ushindi wa Simba wa magoli 4-1 dhidi ya AS Vita kwenye uwanja wa Mkapa Dar es salaam.

“Niwaombe radhi waheshimiwa wabunge, lakini mtakubaliana nami Pasaka ya mwaka huu ilikuwa nzuri sana hasa baada ya mtu kupigwa bao 4-1, nashindwa kujizuia kumpa nafasi mbunge wa Kinondoni (Abbas Tarimba) asiulize swali,” amesema Spika Job Ndugai.

Aidha mbunge wa Kinondoni Abbas Tarimba naye akajibu kuwa amepokea kijembe hicho huku wakiwashauri Yanga SC kuitumia kama mfano ili kuendelea kuitangaza Tanzania kimataifa.

“Naona kijembe kimeingia sawasawa lakini na mimi ni wapongeze kwasababu Simba SC wameisaidia Tanzania kuweza kuonekana vizuri na ule utaratibu wa kuitangaza Tanzania “Visit Tanzania” kusema kweli ni jambo linalofaa kuigwa na wenzetu wa Yanga  pindi watapofanikiwa kuingia kwenye mashindano haya,” amesema Abbas Tarimba.