Ijumaa , 7th Mei , 2021

Mshambuliaji nyota wa zamani wa Yanga, Ramadhan Kampira, amejinasibu timu yake kuibuka na ushindi dhidi Simba kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa utakaochezwa Jumamosi Mei 8, 2021 majira ya saa 11:00 jioni.

Haruna Niyonzima mchezaji mzoefu kwenye dabi ya kariakoo

''Watu wanamtazamo tofauti sana juu ya kikosi chetu, wanaamini Simba wapo juu sana dhidi yetu lakini ukweli si huo, sisi tuna timu bora imara na ya ushindani, sisi siyo 'underdog' kama wengine wanavyodhani, tunakwenda kuibuka na ushindi kesho panapo majaliwa'' alisema Kampira.

Kampira aliongeza ''ujue dabi ni dabi tu, haijalishi mafanikio na ubora wa timu kwenye mechi nyingine,unapokuwa mchezaji wa timu hizi unapaswa kuipambania timu yako hadi nukta ya mwisho ndiyo maana mara nyingi mechi hizi hutoa matokeo tofauti na matarajio ya wengi.

Kampira aliyepata kuichezea Yanga katika miaka ya 1970 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1980 kwa sasa ni mjumbe wa kamati ya ufundi wa timu hiyo,ameonekana kukiamini sana kikosi chake cha sasa kufuatia mchezo mzuri waliouonesha dhidi ya Tanzania Prisons na Azam licha ya kufungwa.

Simba na Yanga wanakutana jumamosi katika uwanja wa Hayati Benjamin William Mkapa ikiwa ni mechi yao ya 108 tangu walipoanza kukutana katika mashindano yote 1965, huku takwimu zikionesha Yanga amepata ushindi mara 37 Simba mara 32 na sare 38.