Jumamosi , 16th Dec , 2017

Klabu ya Singida United imewekeza kwa vijana baada ya kuwanasa vijana wanne waliokuwa na timu ya taifa ya vijana wa umri chini ya miaka 17 Serengeti Boys iliyoshiriki michuano ya AFCON 2017 nchini Gabon.

Singida United imeeleza kuwa hatua hiyo nni mipango ya klabu katika kusaidia vijana wenye vipaji na vimeshaonekana katika ngazi ya taifa.  Pamoja na hilo usajili huo umeelezwa kuwa ni mipango ya maboresho ya kikosi hicho kuwa na timu imara itakayodumu kwa muda mrefu.

Vijana waliosajiliwa ni aliyekuwa nahodha wa Serengeti Boys, Issa Makamba ambaye anacheza nafasi ya kiungo wa kati, mshambuliaji Assad Juma, mlinzi  Ally Ng’azi na mshambuliaji Mohamed Abdallah.

Wachezaji hao wanne wamesaini mkataba wa miaka mitatu kila mmoja na wamelipwa Ada ya usajili (Signing fee) pamoja na stahiki zao zingine ambazo wataendelea kulipwa ikiwemo mishahara.

Katika usajili huu wa dirisha dogo Singida United imeongeza nyota kadhaa ambao ni Daniel Lyanga kutoka Fanja ya Oman, mwingine ni Lubinda Mundia kutoka Zambia pamoja na mshambuliaji kutoka DRCongo Kambale Salita 'Papy Kambale'.