Akizungumza jijini Dar es salaam, Kocha msaidizi wa kikosi hicho, Salum Mayanga amesema wachezaji hao hawataingia kucheza mechi hiyo kutokana na kuwa katika maandalizi ya mechi ya Nani Mtani Jembe inayotarajiwa kuchezwa Desemba 13 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam ambapo amesema kikosi chake kitakachoivaa Burundi hapo kesho kimejiandaa ili kuweza kushinda mechi hiyo.
Mayanga alikitaja kikosi kitakachoivaa Burundi kesho kuwa ni Walinda Mlango Aishi Manula na Benedicto Chinoko huku wachezaji wakiwa ni Abubakar Mohamed, Miraj adam, Joram Mgeveke, Andrew Vicent, Gabriel Michael na Emmanuel Semwanda.
Wengine ni Edward Charles, Pato Ngonyani, Abdi banda, Adam poo, Hussein Moshi, Shiza Ramadhan, Omary Nyenze, Kelvin Friday, Afrey Juma, Salum Mbonde, Atupele Green na Rashid Yusuph.
Kwa Upande wake, Mratibu wa kikosi hicho, Martin Chacha amesema kiingilio katika mechi hiyo kitakuwa ni shilingi Elfu tatu kwa viti vyote ambapo amesema wameamua kuweka kiwango cha chini ili kila mtanzania aweze kushuhudia mechi hiyo ya maadhimisho ya miaka 53 yas Uhuru wa Tanzania Bara.
Chacha amesema kikosi cha Timu ya Burundi kinatarajiwa kuwasili leo jioni ambapo kitafanya mazoezi Uwanja wa Taifa ikiwa ni sehemu ya kujiandaa na mechi ya kesho dhidi ya Stars.