Jumatatu , 3rd Apr , 2017

Nahodha wa klabu ya Simba inayosaka ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara msimu huu Jonas Mkude, amewatoa hofu mashabiki wa timu na kuwaeleza kuwa bado nafasi ya ubingwa ipo upande wao.

Jonas Mkude

Akizungumza baada ya kipigo walichokipata jana dhidi ya Kagera Sugar katika dimba la Kaitaba Bukoba, Mkude amesema bado ligi haijamalizika, hivyo wapenzi na mashabiki wasikate tamaa mapema bali wasubiri hadi mwisho wa msimu kwa kuwa Simba bado ina mechi za ushindi na lolote linaweza kutokea kwa wapinzani wao Yanga ambao ndiyo wanafukuzana nao katika mbio hizo.

"Ligi bado haijamalizika, kwahiyo mashabiki waendelee kutusapoti, nafasi ya ubingwa bado ipo Simba" Amesema Mkude.

Akizungumzia kufungwa na Kagera, amesema huo ndiyo mchezo wa soka na hayo ndiyo matokeo hivyo hawana cha kufanya kwa kuwa matokeo tayari yamekwishatokea.

Amesema kwa kawaida wao kama wachezaji huingia katika mchezo wowote wakiwa na nia ya kushinda, na hufanya jitihada zote dimbani kupata ushindi lakini wakati mwingine mambo hushindikana kwa kuwa mchezo wa soka una matokeo ya aina tatu yaani kushinda, kushindwa na kutoka sare.

Baada ya kufungwa 2-1 jana na Kagera Sugar, Simba imebaki nafasi ya 2 ikiwa na pointi 55 nyuma ya Yanga yenye point 56