Jumatatu , 15th Mei , 2017

Nahodha wa timu ya Serengeti Boys, Issa Abdi Makamba ameondolewa kwenye Kikosi kinachotarajiwa kushuka leo dimbani kuvaana na Mali katika michuano ya AFCON U-17 huko Libreville nchini Gabon baada ya kupata mpasuko wa mguu wakati akifanya mazoezi.

Kikosi cha Serengeti Boys

Hayo yamebainishwa na Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Shime na kusema ni jambo la kusikitisha kwa kumkosa Nahodha huyo katika michuano ya mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 katika hatua ya makundi kutokana na majeruhi aliyoyapata wakati akishirikiana mazoezi na wenzake hivyo hatoweza kushiriki michuano yote pamoja na jina lake kuondolewa katika kikosi cha wachezaji.

"Ni jambo la kusikitisha kidogo kwamba Nahodha wetu Issa Abdi Makamba alipata mpasuko wa mguu juzi mazoezini kwa bahati mbaya akiwa pekee yake kabisa…Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa madaktari wangu wamesema kwamba hatoweza kushiriki mashindano haya na jina lake tumeliondoa katika mashindano tayari nafasi yake imeshachukuliwa na mtu mwingine kwa sababu tulikuwa na wachezaji wa akiba". Alisema Shime

Aidha, Shime aliendelea kwa kusema “Imekuwa bahati mbaya kwetu, bahati mbaya kwa Issa Abdi amepambana kwa miaka miwili kuiongoza hii timu kuhakikisha inafikia hapa ambapo imefika lakini tunaamini mchango wake ni mkubwa sana na kwa sababu bado yupo ndani ya kikosi anaendelea na majukumu yake kama Kapteni kuhamasisha na kuongoza wenzake bado tunampa pole Issa Abdi tunaamini kabisa wachezaji wanatakiwa kupigana kwaajili yake”.