Jumatatu , 2nd Jul , 2018

Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) limeomba Shirikisho la Soka Duniani FIFA kuitazama upya sheria yake ya “Fair Play“ baada ya timu yao kuondolewa kwa sheria hiyo katika hatua ya makundi Kombe la Dunia nchini Urusi.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Senegal baada ya mechi yao dhidi ya Colombia Juni 28, 2017.

Japan na Senegal zilililingana alama zao pamoja na tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa ambapo FIFA ikatumia sheria hiyo ya 'Fair Play' ambayo hutazama upande wa nidhamu hivyo Seneal kuondolewa kutokana na kuwa na kadi nyingi za njano. Senegal  ndio ilikuwa nchi ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia kuondolewa kwa sheria hiyo.

“Huko mbeleni kukitokea mazingira kama haya inatakiwa watafute aina nyingine ya maamuzi, ni vizuri kwa FIFA kuanzisha sheria hii lakini maswali ni kwamba itatatua matatizo yote?, kwasababu baada ya mchezo hakuna chochote kilichotokea kwa Japan au Senegal“. Alisema Msemaji wa FSF, Kara Thioune.

Katika sheria hiyo mpya iliyotumiwa na FIFA inaondoa alama moja kwa kadi ya njano huku kadi nyekundu iliyopatikana kwa kadi mbili za njano inaondoa alama tatu na kadi nyekundu ya moja kwa moja inaondoa alama nne kwa timu husika.

FSF pia imewasilisha barua yao kwa FIFA wakilalamikia kuhusu mazingira hayo ya utoaji wa ushindi kwa Japan ambao umewapa nafasi ya kuingia katika hatua ya 16 bora na Senegal kuyaaga mashindano.