Jumatano , 30th Dec , 2015

Wizara ya Habari, michezo, sanaa na utamaduni imetoa baraka zake kwa Mchezaji wa kimataifa Mbwana Ally Samatta katika ushiriki wake katika kuwania tuzo ya Mchezaji bora wa ndani wa Africa huku akitarajia kujiunga na klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji.

Waziri wa michezo Nape Nnauye amesema mafanikio aliyofikia Samatta ni juhudi aliyonayo katika kuitambua kazi yake hivyo kwa watanzania pia wanatakiwa kumuunga mkono kwani tuzo anayowania Samatta ni ya watanzania wote.

Nape amesema atahakikisha michezo inakuwa shughuli rasmi ya uchumi ya kuwaingizia kipato wachezaji.

Kwa upande wake Samatta ameishukuru Serikali kwa kupitia Wizara husika pamoja na watanzania kwa kuendelea kumuunga mkono na kuahidi kuendelea kuitangaza Tanzania katika ramani ya soka.

Samatta amesema amejifunza mengi katika soka la kimataifa na bado ataendelea kujifunza.

Samatta anatarajia kuondoka hivi karibuni kuelekea nchini Ubelgiji kwa ajili ya kuendelea na mazungumzo na klabu ya KRC Genk ya nchini humo ambapo anasubiri imalizane na klabu yake ya TP Mazembe ya DR Congo ili kuweza kusaini mkataba wa kuanza kazi rasmi ya kuitumikia klabu hiyo.