
Lionel Messi akionekana kusikitika baada ya matokeo mabaya.
Nyota huyo wa Argentina mwenye umri wa miaka 33, anamaliza mkataba wake majira ya joto msimu huu na hadi sasa bado hajaafiki kama ataongeza kandarasi au ataondoka camp nou.
Inasemekana huenda Messi akafikia muafaka wake wiki mbili zijazo wakati maamuzi makubwa ya vilabu vikubwa barani Ulaya yatakapotolewa kuelekea dirisha kubwa la usajili.
Messi alituma faksi kwa Barca mwezi Agosti 2020 akisema anataka kutumia kifungu katika mkataba wake ambacho kinamruhusu aondoke bure kandarasi yake itakapo malizika. Lakini badala yake klabu ya Barcelona ilisema kifungu chake cha kutolewa cha euro milion 700 (£624m) kitalazimika kutimizwa kama anataka kuondoka.
Kwa upande wa kocha wa Barcelona, Ronald Koeman alisema ana matumaini Messi hajacheza mchezo wake wa mwisho kwa Barca kwenye Uwanja wa Nou Camp kufuatia kichapo cha 2-1 na Celta Vigo Jumapili iliyopita, na ataendelea kuwepo Barcelona hivyo akaamua kumpa likizo mapema na kutomjumuisha kwenye mchezo wa mwisho wa msimu dhidi ya Eibar wa jana jumamosi.