Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Samatta akitambulishwa na viongozi wa Genk hapo jana.
Hii leo baadhi ya mashabiki na wadau wa soka nchini wametoa maoni yao tofauti juu ya mafanikio hayo ya Samatta wakitaka iwe chachu kwa wachezaji wengine lakini pia wakitaka wawe na nidhamu na kujitambua.
Suala la Samatta kupata nafasi ya moja kwa moja kujiunga katika klabu hiyo ya Ubelgiji ambayo ina historia ya kutoa wana ndinga kadhaa ambao hivi sasa wanatamba na vilabu mbalimbali barani Ulaya kama kina Christian Benteke, Oligi na wengineo wengi imekuwa gumzo kwa mashabiki na wadau mbalimbali wa soka si tu hapa nchini lakini pia ukanda wa Afrika Mashariki na kati.
Samatta ambaye ni mfungaji bora wa ligi ya mabingwa barani Afrika kabla ya kutua Genk uhamisho wake ulikuwa gumzo hasa baada ya kuwepo kwa mgongano wa kimaslahi na mitazamo baina ya mmiliki wa klabu yake ya zamani ya TP Mazembe Moise Katumbi na kambi ya Samatta.
Mvutano huo ulitokea hasa baada ya tajiri huyo wa migodi ya Shaba kutaka awali mtanzania huyo akacheze klabu ya Standard Liege ya Ubelgiji ama St. Etienne ya Ufaransa kitu ambayo Samatta mwenyewe hakukubaliana nacho kwani tayari mawazo yake yalikuwa kwa klabu ya KRC Genk huku awali kukienea tetesi kuwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba tayari alikuwa ameshasaini mkataba wa awali.
Lakini yote kwa yote kinda huyo ambaye amejijengea umaarufu barani Afrika hasa nchini Congo DR amefanikiwa kutimiza ndoto zake za safari ndefu ya kucheza ligi kubwa barani Ulaya huku akiwa na mtazamo chanya wa kucheza ligi kubwa zaidi zinazotazamwa zaidi ulimwenguni kama EPL, Seria A, La Liga na Bundesliga.
Wadau wengi wa michezo wamekuwa wakimpongeza Samatta kwa mafanikio hayo na pia wakisema hilo liwe funzo ama darasa tosha kwa wachezaji wengine wakitanzania wenye ndoto kama za Samatta ambaye mafanikio yake yamechangiwa na bidii, utayari, nidhamu na kujitambua kwake kitu ambacho wadau hao wamedai ni cha msingi na kinapaswa kuigwa na chipukizi wengine ambao wanataka kufanikiwa kama Samatta.
Wakati huo huo Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi naye amempongeza mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” Mbwana Samatta kwa kufanikiwa kujiunga na klabu ya Racing Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini Ubeligiji.
Malinzi amempongeza Samatta kwa kupata nafasi ya kucheza ligi kuu ya Ubeligiji baada ya kusaini mkataba wa miaka mitatu na nusu kuichezea RC Genk inayoshika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini humo.
Kufuatia kupata nafasi hiyo, Malinzi amemtaka Samatta kujituma kwa nguvu zake zote na uwezo wake wote ili kuendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika nyanja za kimataifa na kwa sasa barani Ulaya.
Aidha Malinzi amewataka wachezaji wengine kujituma na kutumia nafasi wanazozipata katika vilabu vyao kwa kufanya vizuri na kupata nafasi ya kuvuka kwenda kucheza soka la kimataifa nchi za nje.