
Mlinzi wa zamani wa Simba na Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars Boniface Pawasa,ametaka kocha wa Simba Mwingereza Dylan Kerr apewe muda zaidi wa kukijenga kikosi cha timu hiyo.
Mlinzi huyo aliyecheza robo fainali ya klabu bingwa ya soka Barani Afrika mwaka 2003 akiwa na Simba,amesema Simba ina wachezaji wengi vijana ambao bado wanajengwa hivyo ni wakati wa kocha wa timu hiyo kuachwa afanye kazi kwa muda mrefu.
Pawasa amesema kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakisajili wachezaji na kumletea Mwalimu na pindi wachezaji hao wakiwa hawaendani na mfumo lawama zote urudi kwa mwalimu.
Akilinganisha na wachezaji wa Yanga,Pawasa amesema wachezaji wa Yanga wamekaa kwa muda mrefu akitolea mfano wa mabeki Nadir Haroub Canavarho na Kelvin Yondani wameimarisha safu ya ulinzi ya timu kwa zaidi ya miaka 5 sasa,tofauti na Simba inayokuwa kila wakati inabadili wachezaji.
"Ninaamini Simba inaweza,ina vijana wazuri lakini ipewe muda zaidi" alisema Pawasa.
Simba hadi sasa imeshinda mechi saba,na kupoteza mbili dhidi ya Yanga na Prisons katika mechi 9 ilizocheza,huku ikiwa nafasi ya 4 kwenye msimamo wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara 2015/2016.