Mlinzi wa kati wa Klabu ya Yanga, Bakari Nondo Mwamnyeto (Pichani) akiwa mazoezini na Klabu yake hiyo mpya aliyojiunga nayo katika dirisha hili la usajili.
Mgunda ambaye pia ni kocha msaidizi katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania, amesema kuwa yeye ni kama mzazi na anamfahamu Mwamnyeto kwa muda mrefu na kwa kuwa alimfundisha kwa miaka mitatu iliyopita, hivyo hakuna siri kwamba alishamuelekeza namna ya kuishi ili afikie mafanikio yake.
Akizungumza na Kipenga, Mgunda amesema kuwa alimwambia wazi Mwamnyeto kuwa maisha ya Coastal Union yalishapita na ayaache huko na sasa anapaswa kuiangazia Yanga ambayo ipo tofauti na Timu yake hiyo ya zamani.
Ameenda mbali zaidi kwa kusema kuwa ameingia kwenye kikosi ambacho kina matumaini makubwa na uwepo wake ,hivyo anahitaji kupambana na kujiimarisha maradufu ili adhihirishe ubora wake ambao hana mashaka nao.
KWA NINI ANAWEZA KUYUMBA ?
Kwa misimu mitatu iliyopita, Klabu ya Yanga imekua ikisuwasuwa katika michuano mbali mbali, na pia haijatwaa taji la aina yoyote, hivyo shinikizo na matarajio ni makubwa zaidi kwa wanachama na mashabiki wa Timu hiyo, hivyo inaweza kumfanya Mwamnyeto akashindwa kuonyesha kiwango chake.
Pia anakutana na wachezaji wa aina tofauti, alishazoeana na Ibrahim Ame ambaye na yeye alitimkia katika klabu ya Simba,ikumbukwe wawili hawa walipata muda wa kucheza kwa pamoja na kujenga ukuta mzuri katika Klabu ya Coastal Union,lakini sasa atacheza na Lamine Moro,Juma Makapu ambao haitoi taswira halisi kama watakua na muunganiko kwa haraka kiasi gani.
INAWEZEKANA AKAFANIKIWA HARAKA?
Ndio, Mwamnyeto ni mchezaji mwenye umri mdogo, ameshaichezea Timu ya Taifa, na kizuri zaidi huenda kuondoka kwa wakongwe kama Kelvin Yondan, ambaye mustakhabali wake haujawa mzuri ndani ya Yanga, lakini pia Ally Mtoni Sonso aliyetupiwa virago, huenda ukampa mwanya mlinzi huyo kuwa na uhakika wa namba ambao utampa nafasi ya kucheza mara kwa mara .
Pia usajili mpya huenda ukajenga kikosi imara ambacho kitapunguza udhaifu ambao ungesababisha Timu kutegemea zaidi safu ya ulinzi kufanya kazi ya ziada.
Usajili wa wachezaji kama Zawadi Mauya katika idara ya kiungo, inaweza ikawa chachu ya ulinzi wa safu yao kwa kuwa ni mchezaji mwenye uwezo wa kuilinda safu ya mwisho ya Yanga.