Jumanne , 19th Mei , 2015

Kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mholanzi Mart Nooij amemrejesha nyumbani kiungo Said Juma ‘Makapu’, siku moja baada ya timu hiyo kupoteza mchezo wa kwanza kombe la COSAFA.

Katika taarifa yake mkuu wa idara ya Habari na mawasiliano ya shirikisho la soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto amesema kiungo huyo wa mabingwa wa Tanzania, Yanga SC ameondoka leo ambapo ameshindwa kuichezea Taifa Stars katika kombe la COSAFA kutokana na maumivu ya mgongo na anarejea nyumbani kwa ajili ya vipimo zaidi na matibabu. .

Makapu hakuweza kabisa kufanya mazoezi na Taifa Stars tangu afike wiki iliyopita, kutokana na maumivu aliyoyapata katika mchezo wa mwisho wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara dhidi ya Ndanda FC mjini Mtwara mwanzoni mwa mwezi.

Stars jana imefungwa bao 1-0 na Swaziland katika mchezo wa kwanza wa kundi B kombe la COSAFA uwanja wa Royal Bafokeng Sports Palace mjini hapa.

Matokeo hayo yanaiweka Stars katika mazingira magumu ya kwenda Robo Fainali - baada ya Madagascar kuifunga 2-1 Lesotho katika mchezo wa kwanza.