Jumapili , 28th Jun , 2015

Kocha mkuu mpya wa Coastal Union mganda Jackson Mayanja amesema atafanya mabadiliko makubwa katika kikosi cha timu hiyo ili kukipa ubora utakaokifanya kiweze kutisha msimu ujao wa Ligi kuu Soka Tanzania Bara.

Kocha Mpya wa Coastal Union, Jackson Mayanja

Katika taarifa yake, Mayanja amesema, kwa sasa yupo nchini Uganda kwa ajili ya mapumziko lakini anatarajia kuwasili Tanga Jumatatu tayari kwa kuanza kibarua kipya.

Mayanja amesema,ameshawakabidhi mahitaji yake na kuwaambia kuanzia Julai mosi ataanza mazoezi ili kukiweka kikosi hicho tayari kwa Ligi kuu msimu ujao.

Mayanja amesema, Coastal ni timu nzuri na aliiona msimu uliopita ilikuwa imara lakini inahitaji kuboreshwa zaidi na huu ni wakati wa usajili na kuna wachezaji wataondoka ambapo kikubwa amewaambia wawe makini kwa kuhakikisha wanapata wachezaji wengine bora zaidi.

Mayanja ambaye aliwahi kuzinoa Kiyuvu Fc ya Rwanda, Timu ya Mamlaka ya mapato ya Uganda URA, Vipers Fc, Bunamwaya na KCC zote za Uganda amesaini mkataba wa miaka miwili kuifundisha timu ya Coastal Union baada ya kutimuliwa Kagera Sugar aliyokuwa anaifundisha hapo awali.