Timu ya Biashara FC ya mkoani Mara inaongoza kundi C ikiwa na alama 27 na leo itakuwa mwenyeji wa Transit Camp ya Dar es salaam. Biashara inahitaji kushinda ili kuzikimbia timu za Alliance Schools na Dodoma FC zenye alama 25.
Alliance Schools inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 25 na leo itakuwa nyumbani kuikaribisha JKT Oljoro huku ikiwa inahitaji ushindi ili kuikimbia Dodoma FC yenye alama 25 pia huku pia ikiomba Biashara FC ipoteze ili iweze kuongoza kundi.
Timu nyingine yenye nafasi ni Dodoma FC ambayo yenyewe inategemea matokeo ya ushindi pekee ili kupanda ligi kuu ambapo leo itakuwa dimbani kucheza na Toto African.
Mechi zote za leo zitachezwa muda mmoja ambao ni saa 10:00 jioni ili kuepusha vitendo vya upangaji wa matokeo. Tayari timu za Coastal Union, KMC na JKT Tanzania zimeshapanda ligi kuu.


