Jumanne , 5th Jan , 2016

Kocha msaidizi wa timu ya soka ya Ndanda FC ya mkoani Mtwara,Ngawina Ngawina ametangaza kubwaga manyanga baada ya kushindwa kuvumilia shinikizo kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo la kumtaka ajiuzulu na kumuacha kocha mkuu Amimu Mawazo

Wachezaji wa timu ya Ndanda Sc ya mkoani Mtwara, wakipokea maelekezo kutoka kwa makocha wao, Hamimu Mawazo (Kocha Mkuu) na Ngawina Ngawina (Msaidizi).

Kocha msaidizi wa timu ya soka ya Ndanda FC ya mkoani Mtwara,Ngawina Ngawina ametangaza kubwaga manyanga baada ya kushindwa kuvumilia shinikizo kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo la kumtaka ajiuzulu na kumuacha kocha mkuu Amimu Mawazo.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Mtwara, Ngawina amesema amekuwa akiandamwa na maneno makali kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo ya kumtaka afanye hivyo na kwa kulinda masilahi ya timu ameamua bora ajiuzulu ili kuhepusha shari.

Kwa upande wake, katibu wa klabu hiyo, Selemani Kachele alipoulizwa juu ya taarifa hizo amesema amezisikia tu kupitia vyombo vya habari lakini bado hajapata taarifa rasmi kutoka kwa kocha huyo ambaye amedumu na klabu hiyo tangu ilipopanda ligi kuu.

Katika mchezo wa ligi kuu uliowakutanisha Ndanda na JKT Ruvu katika uwanja wa Nangwanda Sijaona tarehe 26, Desemba 2015, Mtwara, mashabiki wa klabu hiyo walisikika kwa kipindi kirefu kumshambulia kocha huyo kwa maneno wakimtaka aachie ngazi kwa madai kuwa anaigawa timu na kutokuwa na maelewano mazuri na kocha mkuu Amimu Mawazo.