Alhamisi , 9th Mar , 2023

Nchi sita zimewasili jijini Dar es Salaam tayari kwa mashindano ya Riadha ya Vijana chini ya miaka 18 na 20 ' EAAR U 20 & 18 Championship' yatakayoanza kutimua vumbi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Machi 10-11 mwaka huu.

Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza saa tatu asubuhi, kwa mbio za mita 100 wasichana.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Lwiza John, nchi zilizowasili jijini Dar es Salaam ni pamoja na Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Somalia, Zanzibar na wenyeji Tanzania Bara.

Lwiza, alisema mashindano hayo yanatarajiwa kuwa na ushindani wa hali ya juu na kuwaomba wakazi wa jiji la Dar es Salaam na vitongoji vya jirani kujitokeza kwa wingi, kwani kutakuwa hakuna kiingilio na kwa kufanya hivyo, kutawatia hamasa vijana wa Kitanzania kufanya vizuri na kuipeperusha vema bendera ya Taifa.