Jumatano , 8th Feb , 2017

Nahodha wa Bayern Munich Philipp Lahm ambaye pia ndiye aliyekuwa nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani walipotwaa Kombe la Dunia mwaka 2014, ametangaza kwamba atastaafu soka mwishoni mwa msimu huu

Philipp Lahm

 

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 ametangaza uamuzi huo baada ya Bayern kushinda mechi ya hatua ya 16 bora katika michuano ya Kombe la Ujerumani dhidi ya Wolfsburg, usiku wa jana, ikiwa ni mechi yake ya 501 kuwachezea vinara hao wa Bundesliga.

"Ninaweza kuendelea na mtindo wangu wa uongozi, kujitolea kila siku, kila kipindi cha mazoezi, hadi mwisho wa msimu. Ninaweza kuendelea kufanya hayo msimu huu lakini si zaidi ya hapo," amesema.

Lahm, alicheza mechi yake ya kwanza katika kikosi cha wachezaji wakubwa wa Bayern mwaka 2002 na ameshinda mataji saba ya Bundesliga akiwa na klabu hiyo, pamoja na Kombe la Ligi ya Klabu Bingwa Barani Ulaya.

Alitangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa baada ya kushinda Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka 2014.