Jumanne , 27th Nov , 2018

Klabu ya Mtibwa Sugar imerejea na moto mkali kwenye michuano ya kimataifa baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Northern Dynamo ya Shelisheli katika uwanja wa Chamazi jijini Dar es salaam.

Wachezaji wa Mtibwa Sugar wakifurahia bao

Mchezo huo ulikuwa wa kuvutia katika dakika zote 90 huku Mtibwa Sugar ikionekana kuwa na kiwango kizuri, ambapo mabao yake yakifungwa na Japhary Kibaya katika dakika ya 13, 36 na 58 pamoja na Riphat Khamis katika dakika ya 90+1.

Mtibwa Sugar imeweka rekodi ya kupata ushindi mkubwa katika michuano hiyo kwenye ardhi yake ya nyumbani huku mchezaji, Japhary Kibaya akiweka rekodi ya kufunga hat-trick yake ya kwanza katika michuano mikubwa ya vilabu barani Afrika.

Ushindi wa Mtibwa Sugar katika mchezo huo unaipa nafasi kubwa ya kusonga mbele katika hatua ya pili, endapo itapata matokeo ya ushindi, sare au kufungwa chini ya magoli 4 kwenye mchezo wa marudio utakaochezwa Disemba 2 nchini Shelisheli.