Ijumaa , 4th Sep , 2015

Kuelekea katika mchezo wa kuwania kucheza fainali za SAFCON kati ya Timu ya Taifa ya Tanzania na Super Eagles ya Nigeria, kocha wa timu ya Taifa Stars Charles Boniface Mkwasa amesema, wamejipanga kufanya vizuri.

Mkwasa amesema, wanajua wanakutana na timu ngumu lakini watajitahidi kufanya vizuri ili kuleta heshima katika ardhi ya Tanzania na ushindi katika mechi hiyo ina umuhimu na utakuwa ni mwanzo wa kufanya vizuri katika mechi zilizo mbele yao.

Mkwasa amesema, watatumia sehemu ya mgogoro uliopo kwa wapinzania wao Super Eagles chini ya kocha wao Sunday Oliseh ili kuweza kufanya vizuri katika mchezo huo kwani wanaamini wakianza vizuri mwanzoni mwa mchezo watamaliza vizuri na kuweza kushinda.

Naye mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa Stars Makumbi Juma amesema, wachezaji wanatakiwa kujitoa katika timu ya taifa zaidi ya kwenye vilabu nyao hususani wachezaji wanaovitumikia vilabu vya nje.

Makumbi amesema, kwa upande wa mashabiki wanatakiwa kuacha ushabiki wa Simba na Yanga na kuweka nguvu zao pamoja kwa ajili ya kuipa sapoti timu yao ya Taifa katika mchezo wa hapo kesho na mingine iliyopo mbele yao.