Ijumaa , 9th Feb , 2018

Nyota wa Chelsea Eden Hazard amesema Chelsea inaweza kuiondoa Barcelona kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya ila tatizo ni moja tu, Barcelona ina mchezaji wa dunia nyingine.

Akiongea kwenye mahojiano na Television moja Hazard ameeleza kuwa pamoja na mwenendo wao kuwa sio mzuri sana lakini wana uwezo wa kushinda mchezo wao wa hatua ya 16 bora dhidi ya Barcelona.

"Wana mchezaji ambaye sio kutoka ulimwengu huu, Lionel Messi na msimu huu wako vizuri tofauti na msimu uliopita, lakini mchezo wa soka sio wa mtu mmoja na namna timu itakavyocheza vizuri kwahiyo hata sisi tunaweza kucheza vizuri na kushinda'', amesema.

Chelsea itaikaribisha Barcelona Februari 20 kwenye mchezo wa kwanza wa raundi ya 16, kabla ya timu hizo kurudiana nchini Hispania Machi 14.