Jumatano , 7th Oct , 2020

Bodi ya Ligi Kuu ya Mpira wa miguu nchini TPLB imefanya mabadiliko ya ratiba ya mchezo wa Ligi Soka Tanzania Bara (VPL), kati ya Yanga dhidi ya Simba uliotarajiwa kuchezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam tarehe 18 Oktoba, umesogezwa mbele hadi Novemba 7 mwaka huu.

Mchezaji wa Simba Clatous Chota Chama akijaribu kuwatoka wachezaji wa Yanga SC

Taarifa hiyo imetolewa leo Oktoba 7, 2020 kupitia kurasa rasmi za mitandao ya kijamii ya bodi hiyo, ikielezea sababu ya mabadiliko hayo ni kuepuka uwezekano wa kukosekana kwa baadhi ya wachezaji katika vikosi hivyo, ambao wanawakilisha mataifa yao katika michezo ya kimataifa ya kirafiki kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Mpira wa miguu duniani FIFA.

"Mabadiliko hayo yametokana na uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa vikwazo vya usafiri wa kimataifa baada ya kukamilika kwa michezo ya kimataifa iliyo kwenye kalenda ya FIFA, jambo ambalo linaweza kuathiri vikosi vya klabu hizo mbili" imesema TPLB.

Aidha, kuibuka kwa janga la virusi vya Corona ulimwenguni kumepelekea kuwe na mlolongo wa mabadiliko ya shughuli mbalimbali ulimwenguni ikiwemo michezo.

Mchezo wa watani wa jadi umekuwa na joto kubwa kwa wapenzi wa mpira wa miguu nchini kutokana na historia ya vilabu hivyo na tambo ambazo huibua hisia mbalimbali.