Jumatano , 22nd Aug , 2018

Mabingwa watetezi wa michuano ya Kikapu ya Sprite Bball Kings Mchenga Bball Stars wameendelea kujiweka vizuri kwenye mbio za kutetea ubingwa wao walioutwaa mwaka 2017 baada ya kushinda game 2 kwa pointi 85 dhidi ya 65 za Flying Dribblers.

Wachezaji wa Mchenga Bball Stars na Flying Dribblers kwenye game 2.

Matokeo hayo sasa yamewafanya Mchenga Bball Stars kushinda game mbili mfululizo kwenye 'best of five' ya fainali ya Sprite Bball Kings baada ya kushinda game 1 iliyopigwa Agosti 18 kwenye uwanja wa taifa wa ndani.

Katika mchezo wa leo uliopigwa kwenye viwanja vya Don Bosco Oysterbay mchezaji Baraka Sadick wa Mchenga ameendelea kuwa moto wa kuotea mbali baada ya kuongoza kwa pointi katika game 1 na leo kufanya hivyo tena akifunga pointi 28 kati ya 85 za Mchenga Bball Stars. 

Pia amechukua rebound 9 na kutoa Assist 5. Kwa upande wa Flying Dribblers mchezaji Steve Mtemihonda, amefunga pointi 19 na kuchukua rebound 6 pamoja na kutoa Assist 2. 

Game 3 ya 'best of five' itapigwa Jumamosi Agosti 25, kwenye uwanja wa ndani wa taifa, ambapo kama Mchenga watashinda watatetea ubingwa wao rasmi lakini kama Flying Dribblers watasawazisha basi itasubiriwa game 4.