Jumamosi , 1st Sep , 2018

Klabu ya Mbeya City imeanza vibaya msimu wa ligi kuu Tanzania bara baada ya kupoteza mchezo wa leo kwa kufungwa na Mtibwa Sugar, ambapo sasa imefikisha michezo mitatu bila ya kupata alama yoyote.

Kikosi cha Mbeya City.

Mchezo huo uliopigwa katika uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro, umeshuhudiwa Mtibwa Sugar wakiibuka na ushindi wa 2-1, mabao ya Stamili Mbonde aliyeanza kufunga dakika ya 9 na Ismail Mhesa katika dakika ya 42 huku bao pekee la Mbeya City likifungwa na Eric Kyaruzi dakika ya 48.

Kwa kupoteza mchezo huo, Mbeya City sasa inafikisha mchezo wa tatu bila ya alama yoyote, ikiwa imefungwa mechi zote na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita dhidi ya bao moja pekee ililofunga katika mechi hizo zote.

Mbeya City ilipoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Azam Fc kwa mabao 2-0 kisha kupoteza mchezo wa pili dhidi ya Simba kwa mabao 2-0 katika uwanja wa taifa, Dar es Salaam.

Mpaka sasa inakamata nafasi ya mwisho ikiwa haina alama yoyote pamoja na Tanzania Prisons na Mwadui Fc ambazo nazo hazina alama yoyote baada ya kucheza mechi mbili kabla ya michezo yao ya leo.

Huenda ratiba ngumu ya Mbeya City ya mechi za mwanzo ikawa sababu iliyopelekea matokeo hayo, baada ya kuanza mechi mbili kubwa mfululizo dhidi ya Simba na Azam Fc na kisha mechi ya leo dhidi ya Mtibwa Sugar ambapo mechi zote imecheza katika viwanja vya ugenini.