Jumamosi , 3rd Sep , 2016

Timu ya Mbao FC ya jijini Mwanza, imezidi kudorora baada ya leo kukubali kipigo kingine cha mabao 4-1 toka kwa Mbeya City ya jijini Mbeyakatika uwanja wa CCM Kirumba.

Mbaye wakipata bao dhidi ya Mbao FC

Mbao ambayo imepanda daraja msimu huu, kwa nafasi iliyopatikana baada ya Geita Gold kushushwa daraja, imeonesha kiwango dunia katika mechi zake zote 3 ilizoanza kucheza hali ambayo imeanza kutia shaka kwa mashabiki wa soka, na kuiona kama timu ambayo haitaweza kuhimili mikiki mikiki ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Magoli ya Mbeya City leo yamefungwa na Rafael Daud aliyefunga magoli mawili, huku mengine yakifungwa na Ramadhan Chombo na Omary Ramadhani.

Baada ya mechi hiyo, EATV imezungumza na makocha wa timu zote mbili pamoja na mashabiki ambao walisema ambapo kocha wa Mbao FC Etiene Ndayiregije amesema timu yake imecheza vizuri lakini bahati haikuwa upande wao huku akiifagilia Mbeya City kwa kucheza vizuri zaidi na kwamba walistahili ushindi huo.

Kocha wa Mbeya City Kinnah Phiri amesema anajisikia vibaya kwa ruhusu bao moja, kwa kuwa lengo lake lilikuwa ni kutoruhusu goli kabisa, lakini ana shukuru kwa kupata pointi 3, pamoja na kuisifia Mbao FC kuwa ina kikosi kizuri kuliko Toto African, na kwamba kitafika mbali.

Mashabiki wa Mbao FC wamemtupia lawama kocha huku wakiipongeza Mbeya City kwa kutumia udaifu wa Mbao FC.

katika michezo mingine iliyopigwa leo, Mtibwa Sugar imeishushia kipigo Majimaji ya Songea, mjini Songea, wakatio JKT Ruvu ikitoka suluhu ya bila kufungana na African Lyon katika uwanja wa Mabatini Pwani huku Kagera Sugar ikijipatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mwafui katika dimb la Kaitaba mjini Bukoba.

Kesho ligi hiyo itaendelea kwa mchezo mmoja utakaozikutanisha Stand United dhidi ya Toto African, katika dimba la CCM Kambarage mjini Shinyanga.

Hadi sasa Mbeya City ipo kileleni ikiwa na point 7 ikifuatiwa na Mtibwa yenye point 6.

Sikiliza hapa sauti za makocha wa Mbao FC na Mbeya City pamoja na mashabiki wa Mbao FC.

Haruna Shamte(katikati) Rajab Zahir (kushoto) wa Mbeya City wakishangilia bao la pili lililofungwa na Omary Ramadhani (Kulia) dhidi ya Mbao FC katika uwanja wa CCM Kirumba leo
Sauti ya Kocha wa Mbao FC Etiene Ndayiregije
Sauti ya Kocha wa Mbeya City Kinnah Phiri
Sauti za baadhi ya mashabiki wa Mbao FC