Jumapili , 3rd Nov , 2024

Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde amekabidhi kwa uongozi wa shule ya sekondari Kiwanja cha Ndege kiwanja cha kisasa cha michezo ya mpira wa kikapu, pete na wavu kama sehemu ya kukuza na kuendeleza vipaji vya wanafunzi wa Jijini Dodoma.

Akizungumza Mavunde amesema, "Katika kuunga mkono jitihada hizi kubwa nimeamua kujenga uwanja huu wa kisasa wa michezo hapa shuleni ili kusaidia kuibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi wa Dodoma".

Mkuu wa wilaya ya Dodoma Alhaj Jabir Shekimweri amempongeza Mbunge Mavunde kwa juhudi kubwa ya kuleta maendeleo Jijini Dodoma na kuwataka wanafunzi kutumia kiwanja kushiriki kwenye michezo ili kujenga afya bora hali itakayowasaidia kujiepusha na makundi mbalimbali ambayo yataathiri maadili yao na afya.

Akitoa salamu zake, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Nchini(TBF) Michael Kadebe, amepongeza juu ya ujenzi wa kiwanja hicho kwa kuwa inaongeza idadi ya viwanja vya mpira wa kikapu Jijini Dodoma na kuahidi kuanzisha kituo cha mafunzo ya vijana Mavunde basketball academy katika shule hiyo kama njia ya kuwaendeleza wanafunzi katika ushiriki wao kwenye mchezo wa kikapu Jijini Dodoma.