Jumanne , 20th Aug , 2019

Afisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema katika utafiti wake barani Afrika amegundua kuwa Simba ni klabu pekee inayoweza kujaza mashabiki elfu 60 uwanjani.

Haji Manara

Akizungumza katika mkutano na wanahabari Jijini Dar es Salaam, Manara amesema kuwa kabla ya kuthibitisha utafiti wake alikuwa akiwaogopa mashabiki wa nchi ya Misri lakini amejiridhisha katika michuano ya AFCON kuwa Simba na mashabiki wake ndiyo wanaoweza kufanya hivyo na si klabu yeyote.

"Naamini mwaka huu kwenye tuzo za mashabiki bora, CAF wataipa Simba, nimekwenda Cairo nimeshuhudia mwenyewe. Nilikuwa na hofu na Wamisri lakini baada ya kuangalia yale mashindano ya AFCON, Simba ndiyo klabu pekee Afrika inayoweza kuingiza mashabiki elfu 60 kwa kila mechi", amesema Manara.

"Suala moja lililobaki kwangu ni kuwahamasisha mashabiki kushangilia kwa dakika zote kama Liverpool, sio kushangilia kwenye magoli pekee. Zile dakika 15 za mwisho kwenye mchezo na AS Vita hapa Dar, ndiyo zilikuwa dakika zangu bora nilizowahi kuzishuhudia Tanzania katika mchezo wa mpira wa miguu", ameongeza.

Aidha Manara amesema kuwa maandalizi ya mchezo wa marudiano kati ya Simba na UD du Songo ya Msumbiji yako vizuri na tiketi zimeshaanza kuuzwa kuelekea mchezo huo. Mchezo huo utapigwa Jumapili, Agosti 25 katika uwanja wa taifa ambapo waamuzi wa mchezo ni raia kutoka nchini Rwanda.

Kuhusu tetesi kuwa anaondoka ndani ya klabu hiyo, Manara amesema kuwa kwa sasa anachotambu yeye ni msemaji rasmi wa klabu ya Simba na kama itakuja kutokea akaondoka itakuwa ni wakakti wake umefika kwani klabu hiyo ni kubwa kuliko jina la mtu.