Man City na Chelsea kuoneshana kazi nchini Ureno

Alhamisi , 13th Mei , 2021

Shirikisho la soka Barani Ulaya ''UEFA'' limethibitisha kwamba Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Chelsea na Manchester City, sasa itachezwa mjini Porto nchini Ureno katika Dimba la Dragao Mei 29 mwaka huu.

Kiungo wa Chelsea, Ngolo Kante akikatiza katikati ya msitu wa wachezaji wa Manchester City kwenye mechi ya EPL waliyokutana hivi karibuni.

UEFA ilitaka kuhamisha fainali hiyo kwenda Wembley nchini England, lakini kulikuwa na hatua za kuzingatia juu ya kuondoa sheria za karantini kwa wafanyikazi 2,000, wafadhili, VIP na Vyombo vya Habari vya kigeni vitakavyoenda nchini humo.

Mwanzoni fainali hiyo ilipangwa kwenye Uwanja wa Ataturk mjini Istanbul, lakini shinikizo liliongezeka la uwanja huo kubadilishwa baada ya Serikali ya England kuweka zuio kwa mashabiki, kwani Uturuki ipo kwenye orodha nyekundu ya nchi zilizo hatarini kwa maambukizi ya Covid-19 na kuwataka mashabiki wasisafiri kwenda kwenye mchezo huo.

Raia wa England wanaorudi kutoka nchi zilizo na orodha nyekundu wanahitajika kujitenga katika hoteli iliyoidhinishwa na Serikali kwa siku 10 hali ambayo ingewanya mashabiki wengi wasisafiri kwenda uturuki tofauti na sasa ilipo hamishiwa nchini ureno.