Jumatano , 6th Apr , 2022

Kocha Mkuu wa Mbeya City FC Mathias Lule amesema kufanya vibaya kwa kikosi chake katika siku za karibuni kunatokana na wachezaji wa klabu hiyo kujisahau.

Kocha Lule raia wa Uganda amesema, asilimia kubwa ya wachezaji wa Tanzania wanapopata matokeo mazuri mfululizo huwa wanajisahau, na kuona wameshamaliza kila kitu, jambo ambalo limeisibu timu yake katika kipindi hiki.

“Tatizo la wachezaji wengi wa vilabu vya Tanzania pale wanapopata ushindi mfululizo basi huwa wanasahau kuendelea kupambana ili wapate ushindi zaidi na zaidi” amesema Kocha Lule

Kabla ya kupoteza mchezo wa April dhidi ya Geita Gold, Mbeya City FC ilipoteza dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wake wa nyumbani kwa kufungwa 1-0.

Kwa matokeo hayo Mbeya City FC ambayo ilikua na mwanzo mzuri msimu huu, inaendelea kuwa katika nafasi ya 05 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 25, zilizopatikana kwenye michezo 19 waliocheza hadi sasa.