Jumatano , 28th Oct , 2015

Ligi kuu ya soka Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea hapo kesho kwa kumalizia mzunguko wake wa tisa kwa michezo miwili kupigwa ambapo Azam FC watakaribishwa na JKT Ruvu uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

Katika mchezo mwingine utakaopigwa hapo kesho, wajelajela Tanzania Prisons wakiwakaribisha African Sports katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Afisa Habari wa Klabu ya Azam FC Jaffary Iddy Maganga amesema, mchezo utakuwa mgumu kwani JKT Ruvu ni wazuri na ni wapinzani kwa muda mrefu.

Maganga amesema, majeruhi waliokuwa nao ambao ni Mudathir Yahya na Farid Mussa hivi sasa wanaendelea vizuri, hivyo kupangwa katika mchezo huo itategemea na kocha huku kocha mkuu Stewart Hall akiwa na kikosi chake uwanjani hapo kesho baada ya kumaliza adhabu ya kadi aliyokuwa akiitumikia.