Jumatano , 2nd Sep , 2020

Uongozi wa Klabu ya Simba umekanusha taarifa zilizoandikwa na kuripotiwa na baadhi ya mitandao ya kijamii na vyombo vya Habari kuwa mshambuliaji wao Meddie Kagere amepigana na Kocha wake Sven Vandenbroeck wakiwa mazoezini si za kweli na zina lengo la kuvuruga amani ya Timu yao.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara.

Mkuu wa Idara wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Haji Manara amesema ndani ya Timu ya Simba kuna amani  na furaha kubwa na hakujawahi kutokea ugomvi wa aina yoyote kama ambavyo taarifa zimeripotiwa.

''Wanasema jana ugomvi uliotokea mazoezini,lakini Simba hawakuwa na mazoezi baada ya mchezo wa ngao ya jamii ,hivyo ni propaganda ya kuvuruga utulivu uliopo ndani na nje ya Simba wakitaka itokee kama upande wa pili yanayoendelea''

''Kama idara ya Habari na Mawasiliano hatutokubali kuona watu wanaandika uzushi kuhusu Klabu yetu na tutachukua hatua kali dhidi ya watakaohusika''

Kumekua na taarifa kuwa Kagere ambaye ndiye mfungaji bora wa Ligi kuu kwa misimu miwili mufululizo aligombana na Kocha baada ya kuhoji kwa nini hapewi nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza .