Jumatano , 6th Dec , 2017

Klabu ya soka ya Kiluvya United ya Mkoa wa Pwani imefanikiwa kupata klabu rafiki inayofahamika kama Tampere inayoshiriki ligi kuu nchini Finland.

Katibu wa klabu hiyo inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Omary Masawilla amethibitisha hilo, ambapo ameeleza kuwa urafiki huo umefanikishwa na mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo.

“Ni kweli tumepata klabu rafiki ya huko Finland inashiriki ligi kuu na wameona sisi tuna mipango mizuri na uwezo wa kupanda ligi kuu hivyo wakaomba tushirikiane katika mambo mabalimbali, tayari mkuu wa mkoa ameshatupa maelekezo na kinachosubiriwa ni wao kuja kukutana na sisi ili kuanza utekelezaji”, amesema Masawilla.

Ushirikiano huo utahusisha maeneo kadhaa ikiwemo  kukuza vipaji, mbinu za uchezaji na benchi la ufundi ili kuinua soka mkoani humo. Ushirkiano huo utaleta manufaa makubwa kwa vipaji vya soka hususani vijana katika mkoa wa Pwani.

Kwa upande mwingne Mkuu wa mkoa ametoa kiasi cha shilingi milioni moja kwa timu hiyo inayoshiriki ligi daraja la kwanza ili kuhakikisha inapunguza changamoto mbalimbali na hatimaye kutimiza lengo la timu kuingia ligi kuu.

Mhandisi Ndikilo ametoa mchango huo baada ya kutembelea kambi ya  timu hiyo iliyopo kwenye shule ya Filbert Bayi wilayani Kibaha. Kiluvya United inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 14 kwenye kundi A ligi soka daraja la kwanza nyuma ya vinara JKT Ruvu yenye alama 23 wakati African Lyon inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 17.