Ijumaa , 15th Dec , 2017

Rais mstaafu wa serikali ya awamu ya nne ya Jamhrui ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameipongeza timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) baada ya kutinga fainali ya CECAFA 2017.

Zanzibar Heroes imetinga fainali baada ya kumfunga 2-1 bingwa mtetezi wa michuano hiyo Uganda kwenye mchezo wa nusu fainali ya CECAFA Senior Challenge uliofanyika jioni ya leo kwenye uwanja wa Moi mjini Kisumu Kenya.

“Nawapongeza Zanzibar Heroes kwa kututoa kimasomaso na kutinga fainali. Nawatakia kila la kheri katika mechi ya fainali waibuke na kombe na watupe raha ambayo Watanzania tumeikosa kwa muda mrefu”, ameandika Dkt. Kikwete kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Twitter.

Rais huyo mstaafu anasifika kwa kupenda michezo na akiwa madarakani amewahi kumlipa mshahara aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kwa wakati huo Marcio Maximo.

Zanzibar Heroes itacheza mchezo wa fainali siku ya Jumapili dhidi ya wenyeji Kenya. Katika michuano hiyo Tanzania iliwakilishwa na timu ya Kilimanjaro Stars ambayo haikufanya vizuri baada ya kuondolewa katika hatua ya makundi ikiwa na alama moja tu.