Kocha Mkuu wa Simba SC, muingereza Dylan Kerr anaweza kuondolewa kazini iwapo hatakuwa na hoja za utetezi za kuiridhisha kamati ya utendaji ya klabu.
Kamati ya utendaji, chini ya Rais, Evans Elieza Aveva inatarajiwa kumuhoji masuala mbalimbali Kerr katika kikao kinachotarajiwa kufanyika hii leo Dar es Salaam.
Kerr anatuhumiwa kwa kushindwa kuifanya Simba SC icheze vizuri na uongozi unaamini kiwango cha timu kimeporomoka kwa kiasi kikubwa kutoka alivyoikuta Julai mwaka jana ilipoachwa na Mserbia, Goran Kopunovic.
Aidha, anashutumiwa kwa ushauri wake mbaya kwa uongozi uliosababisha wachezaji kadhaa wazuri akiwemo Elias Maguli wakaachwa na wakasajiliwa wachezaji wa kiwango cha chini kama Msenegali, Abdoulaye Pape N’daw aliyeachwa Desemba mwaka uliopita.
Kitendo cha Simba kumteua kocha Jackson Mayanja kuwa kocha msaidizi wa Dylan Kerr, kinatafsiriwa na wachambuzi wa soka kuwa huenda mzungu huyo akatimuliwa muda wowote na msaidizi wake Mayanja akapewa timu kwa muda hadi atakapopatikana kocha mwingine.
